Dar es Salaam. Mahakama Kuu imesimamisha kwa muda amri yake ya kuwakamata wakurugenzi wawili wa Kampuni ya Tip Top Connection, Hamis Shaban Taletale maarufu Babu Tale na ndugu yake Idd Shaban Taletale.
Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na naibu msajili, Wilbard Mashauri, Februari 16, 2018 iliamuru Babu Tale na nduguye wakamatwe na kupelekwa kifungoni katika Gereza la Ukonga na Aprili 4, 2018 kwa kushindwa kutekeleza hukumu ya mahakama.
Awali, katika hukumu iliyotolewa na Jaji Agustine Shangwa Februari 18, 2016 iliwaamuru ndugu hao kumlipa fidia ya Sh250 milioni mhadhiri wa Dini la Kiislamu, Sheikh Hashim Mbonde kutokana na makosa ya kutumia mahubiri yake kibiashara bila ridhaa yake.
Kufuatia amri na hati hiyo, Babu Tale alitiwa mbaroni na polisi Mkoa wa Ilala na kuhifadhiwa kituoni hapo kwa siku mbili akisubiri naibu msajili Mashauri kuidhinisha amri yake ya kumpeleka gerezani kuwa mfungwa wa madai, kwa kuwa naibu msajili huyo hakuwepo.
Juzi jioni, Jaji Edson Mkasimongwa alimuachia huru kwa muda kwa kile kinachoelezwa kuwa ni makosa ya amri hiyo na kumtaka afike mahakamani jana na akamwelekeza wakili wake amtaarifu wakili wa mdai afike mahakamani ili kuzisikiliza pande zote.
Hata hivyo, usikilizwaji wa hoja ambazo ziliibuliwa na mahakama yenyewe kuhusiana na amri ya kuwakamata ulikwama kutokana na upande wa mdai kutofika mahakamani.
Badala yake, Jaji Mkasimongwa aliahirisha shauri hilo hadi Juni 8, 2018 na kuagiza upande wa mdai kupewa taarifa ya wito kwa ajili usikilizwaji wa hoja zilizoibulia na mahakama yenyewe.
Pia jaji alisimamisha amri ya kuwakamata hadi Juni 8.
Jaji Mkasimongwa alitoa amri hiyo kufuatia maombi yaliyotolewa na wakili wa Babu Tale, Issa Chombo baada ya usikilizwaji wa shauri hilo kukwama kutokana na upande wa mdai kutofika.
Awali, wakili Chombo aliieleza mahakama kuwa shauri hilo lilipangwa kusikilizwa kama ambavyo ilielekeza juzi, lakini upande wa mdai hadi wakati kesi inaitwa ulikuwa haujafika.
Wakili huyo alieleza kuwa baada ya maelekezo ya juzi ya mahakama, wakili mwenzake aliwasiliana na wakili wa mdai, Mwesigwa Muhingo kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu na kumpigia simu kumjulisha maelekezo ya mahakama ili afike mahakamani.
“Lakini kutokana na mazingira kwamba taarifa zilikuwa ni za muda mfupi, mpaka sasa hivi hawajafika,” alisema wakili Chombo.
“Hivyo haitakuwa busara kuendelea kuieleza mahakama chochote, badala yake tunaomba ahirisho hadi tarehe nyingine ya karibu ili tuwepo pande zote. Sambamba na hilo, tunaomba mteja wetu aendelee kuwa nje hadi tarehe hiyo.”
Jaji Mkasimongwa alikubaliana na maombi hayo na kuahirisha shauri hilo huku akitoa amri ya kusimamishwa kwa muda kukamatwa kwao.
No comments:
Post a Comment