Hivi karibuni Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe aliibua kasoro za vikao vya wabunge wa vyama (party caucus) bungeni kutumika kuua hoja za wabunge.
Kwa mujibu wa Bashe ambaye katika siku za karibuni amekuwa miongoni mwa wabunge wachache wanaoikosoa Serikali inayoongozwa na chama chake, anasema vikao vya mikakati vinavyolenga kuweka msimamo wa chama, vinaua hoja binafsi zenye masilahi ya wananchi.
Badala yake, mbunge huyo anashauri Bunge likubali kufanya mabadiliko ya kanuni zake ili mbunge aruhusiwe kuwasilisha hoja binafsi bila kulazimishwa kupitia kwenye chama chake.
Bashe alikuwa akishiriki kwenye mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, iliyokosolewa vikali na wabunge – wa chama tawala na upinzani, ikiwa ni siku chache tangu Bajeti ya Kilimo kupita kwa masharti, baada ya wabunge wa CCM kukutana kimkakati na hatimaye kuipitisha.
Wakati Bashe akitoa dukuduku hilo, wafuasi mbalimbali wa chama tawala pamoja na upinzani wameungana na mbunge huyo na kusema kuwa vikao hivyo, vya wabunge wa vyama, si muhimu na kwamba vinaweza kufutwa na visiathiri chochote.
Party caucus ya CCM
Hata hivyo, Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa anasema ‘party caucus’ ni kikao cha wabunge wa chama fulani kwa ajili ya kuweka msimamo wa pamoja kuhusu hoja inayotakiwa kupelekwa bungeni.
Msekwa ambaye kabla ya kuwa Spika aliwahi pia kuwa Katibu wa Bunge, anasema ‘party caucus’ katika kila chama ina kanuni na taratibu zake.
Anaongeza kuwa jukumu kubwa la mkutano huo ni kuwaweka wabunge pamoja kwa kwamba ndani ya Bunge kuna siasa za ushindani kati ya kambi ya upinzani na wale wa chama tawala.
Msekwa ambaye pia amewahi kushika nafasi za juu ndani ya Tanu hadi CCM akiwa Katibu Mtendaji Mkuu kwa vipindi tofauti kati ya 1967-1970 na 1977 hadi 1980, anasema kabla ya mbunge kuwasilisha hoja yake bungeni anapaswa kuifikisha kwanza ndani ya ‘party caucus’ ili ijadiliwe na kuona kama kuna uwezekano wa kuungwa mkono na wabunge wote ndani ya chama.
Anaongeza kuwa lengo la mkutano huo hasa kwa chama tawala ni kuhakikisha hoja zao au hoja za serikali zinaungwa mkono na kupita ndani ya Bunge.
Msekwa ambaye amewahi pia kuwa mbunge wa jimbo la Ukerewe kati ya mwaka 1995 hadi 2000 na baadaye kuwa makamu mwenyekiti wa CCM, anasema hoja ya mbunge inapofika ndani ya ‘party caucus’ kama itaonekana haina mashiko na haiwezi kuungwa mkono na wabunge wote basi mbunge husika huambiwa aiondoe hoja yake.
Hoja zilizokwama ‘party caucus’
Katika hoja zilizokwama, huwezi kuacha kutaja ile ya Bashe ya kulitaka Bunge kuundwa kamati teule kuchunguza matukio ya kihalifu yanayofanyika nchini ya utekaji watu, maiti kukutwa kwenye viroba na mashambulizi ya watu, yanayodaiwa kufanywa na watu wasiojulikana.
Hii ni baada ya kiti cha Spika kusema mbunge huyo alitakiwa kuipeleka hoja yake hiyo kwanza kwenye chama chake, ijadiliwe kwanza kabla ya kuiwasilisha bungeni.
Kwa mujibu wa Spika, Kanuni za Bunge zipo na Kanuni za Uendeshaji wa Shughuli za Bunge kwa wabunge wa CCM kama chama tawala zipo, kama ilivyo kwa wabunge wa kambi ya upinzani ambazo zote ni sehemu ya uendeshaji wa shughuli za Bunge.
Spika Job Ndugai anasema Bashe kama mbunge wa CCM, kanuni za wabunge wa CCM zinamtaka aipeleke hoja yake kwenye chama chake kwanza, ikajadiliwe huko na ikikubaliwa Bunge linaweza kuipokea.
Aprili 2012, ‘Party caucus’ ya CCM ilikutana, pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa ilikuwa hoja ya saini 70, iliyokuwa iwasilishwe na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe kuitaka Serikali ya CCM kuwawajibisha mawaziri watano kwa madai ya kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Zitto alitoa muda kwa Serikali kutekeleza hoja yake na muda ulipokwisha bila kufanyiwa kazi, alianzisha kampeni ya kumng’oa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kukusanya saini 70 kama kanuni ya Bunge inavyoelekeza.
Miongoni mwa wabunge walioelezwa kukwepa kusaini ni mbunge (sasa waziri) Hamisi Kigwangalla, lakini kwenye majibu yake mtandaoni Aprili 2012 alisema: “... sioni sababu ya kuiingiza nchi kwenye wasiwasi wa kiutawala kiasi hiki.
“Na kwa kuwa wabunge wa CCM kwenye ‘party caucus’ tulikuwa tayari tumeishaambiwa kwamba kuna mawaziri wameamua kujiuzulu wenyewe (tena siyo wale watano, ni wanane kabisa) kutokana na tuhuma hizo na presha kutoka kwa wabunge wa CCM na wengine, sikuona sababu ya mimi kusaini hoja ya Zitto (ambayo kikanuni ilikuwa imekosewa - kitendo kilichonidhihirishia wazi.”
Party caucus ya Chadema
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje ya Chadema John Mrema anasema ‘party caucus’ ni utaratibu uliozoeleka katika mabunge ya Jumuiya ya Madola lakini lazima ijulikane kwamba haziko juu ya Bunge.
“Bunge lipo kisheria chini ya Ibara ya 100, si sawa vyama kutumia mikutano hiyo kwani inaingilia ibara hiyo ambayo inampa mbunge kuwa huru kusema chochote kwa masilahi ya wananchi wake,” anasema.
Mrema anasema hoja nyingi ziwe za upinzani au chama tawala zinakufa kutokana na mikutano hiyo na kwamba wabunge wanashindwa kujadili na kufanya uamuzi kwa uhuru kwa kuhofia vyama vyao.
Anasema tatizo kubwa lililopo ni mfumo wa chama kimoja tuliorithi ambao mpaka sasa vyama vinaamini chama kikishika hatamu kinapaswa kujilinda hata kama hakuna masilahi katika hoja hizo.
“Vyama vinahodhi wabunge, wanafikiri wabunge ni mali yao wakati ukweli ni kwamba ni mali ya wananchi kwani hao ndiyo waliowatuma kuwawakilisha bungeni,” anasisitiza Mrema.
Serikali ifanye nini?
Kasaka alisema siku zote hoja hujibiwa kwa hoja na si vitisho wala kuisimamisha hoja, hivyo Serikali ina wajibu wa kutafuta majibu sahihi na si kukimbilia katika chama ili kilazimishe mbunge aogope.
Anasema mpaka sasa tunashindwa kutofautisha kati ya Serikali na chama na ukweli ni kwamba wabunge ni wasimamizi wa Serikali na chama chao, hivyo wanapaswa kuwa na uhuru wa utendaji ili inapotokea kosa walisahihishe.
Kasaka alienda mbali zaidi na kutoa mfano wa hoja yake ya Tanganyika kupitia kundi la G55 kwamba hata wakati huo licha ya kwamba viongozi walijenga hoja, lakini ukweli ni kwamba zilipwaya.
“Kinachotakiwa kama kuna hoja isisimamishwe kwa kutumia mfumo wa nje ya Bunge, badala yake wajibu wa Serikali ni kujibu hoja hiyo na si kutoa hofu kwa wabunge wake.
CUF na Party Caucus
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma wa chama hicho, Abdul Kambaya anasema Bunge ni muhimili unaojitegemea hivyo haupaswi kuingiliwa na muhimili mwingine.
Kambaya anaongeza kuwa kitendo cha mikutano hiyo kutoa maelekezo kwa wabunge hakiakisi hali halisi ya chombo hicho, badala yake mijadala itajikita katika uchama zaidi badala ya kuisimamia Serikali kama kazi za wabunge zinavyopaswa kuwa.
“Tanzania hatuwezi kuwa na Bunge huru; hapa nazungumzia vyama vyote yaani chama tawala na upinzani, tumeshuhudia mifano ya wabunge kadhaa ambao walijaribu kutofautiana na misimamo ya vyama vyao wakaonekana wasaliti.”
“Nape Nnauye, Hussein Bashe, Kangi Lugola kutoka chama tawala walipojaribu kuonyesha hisia zao walionekana wasaliti lakini pia Alphan Suleiman wa CUF na wakati Zitto Kabwe akiwa Chadema naye alikumbwa na kadhia hiyo baada ya kutofautiana na chama chake naye alionekana si miongoni mwao. Hii ni hatari sana,” anasisitiza Kambaya ambaye yupo upande unaomuunga profesa Ibrahim Lipumba.
Kambaya anasema kwa mtazamo wake, mikutano hiyo haina umuhimu wowote bungeni na kwamba ni bora isiwepo kabisa kwani kazi ya wabunge ni kuwawakilisha wananchi, hiyo inatosha kabisa kuliko kuwa na maelekezo kutoka katika vyama vyao.
No comments:
Post a Comment